Vyeti vya elimu hutumika kudhibitisha kwamba umemaliza masomo na hukuruhusu kuendelea na masomo zaidi na kuajiriwa. Kupoteza au kuharibu vyeti hivi kunaweza kukusababishia kukosa kazi au fursa ya kuendeleza elimu yako. Cheti cha Kenya cha Elimu ya Sekondari (KCSE) kwa mfano, kinahitajika ili kujiandikisha kuendelea na masomo ya juu kama vile chuo kikuu. Zaidi ya hayo, waajiri wengine huhitaji waajiriwa wao kuwasilisha vyeti vya kitaaluma kama uthibitisho wa kufuzu 

Katika nakala hii, tutaangazia hatua zinazohitajika kuchukuliwa ili kubadilisha cheti cha kitaaluma cha Baraza la kitaifa la mitihani la Kenya (KNEC) kilichopotea au kilichoharibika na kukupa taarifa unayohitaji ili kuhakikisha umepitia mchakato mzuri na unaofaa

Aina za vyeti vinavyotolewa na Baraza la kitaifa la mitihani la Kenya (KNEC)

KNEC inatoa vyeti vifuatavyo vya elimu:

1. Cheti cha Elimu ya Sekondari cha Kenya (KCSE)

Hiki ni cheti ambacho hutolewa kwa wanafunzi waliomaliza elimu yao ya sekondari (Kidato cha 1- Kidato cha 4) nchini Kenya. Cheti hiki hutunukiwa wanafunzi baada ya kufanya mitihani ya kitaifa ya KCSE

2. Cheti cha Elimu ya Msingi cha Kenya (KCPE)

Hiki ni cheti ambacho hutunukiwa wanafunzi ambao wamemaliza elimu yao ya msingi (Darasa la 1 – Darasa la 8) na wamefanya mitihani yao ya KCPE. Wanafuzi wote huhitajiwa kufanya mitihani hii ili kufuzu kwa elimu ya sekondari.

3. Vyeti vya elimu ya baada ya sekondari kama vile Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET), Vyeti vya Biashara na Mafunzo ya Ualimu (TTC).

Kuwasilisha ombi la kubadilisha cheti cha masomo/KNEC

KNEC imefanya mchakato wa kubadilisha vyeti vilivyopotea au vilivyoharibika kuwa  rahisi.

Maombi ya kubadilisha vyeti vya masomo hufanywa kupitia tovuti ya mtandaoni ya KNEC, Mfumo wa Taarifa za Kusimamia Maswali (QMIS). 

KNEC itakupa barua ya Uidhinishaji wa Matokeo ya Mtihani ambayo ni nakala ya cheti pindi ombi lako litakaposhughulikiwa na hati zote zinazohitajika kuthibitishwa

Hati zinazohitajika kuwasilishwa pamoja na ombi lako la kubadilisha vyeti vya KNEC vilivyopotea/ vilivyoharibika.

1. Nakala ya cheti kilichopotea au hati za matokeo: Hati za matokeo zinahitajika kwa mitihani yote isipokuwa mitihani ya KCPE ya miaka 1926 hadi 2012. (Hati za matokeo za mitihani ya KCPE kutoka mwaka wa 2013 vilivyopatikana kutoka kwa tovuti/mfumo wa KNEC vinakubalika).

Unaweza kupata nakala ya hati yako ya matokeo ya KNEC kutoka shule ulikofanyia mitihani yako

2. Hati ya Kiapo ya Kisheria: Hati ya kiapo kutoka kwa wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya.

3. Udhibitisho wa msajili wa umma: Uthibitisho wa kitambulisho cha mwombaji kutoka kwa msajili wa umma.

4. Hati ya Polisi: Hati halisi ya polisi inayoonyesha kwamba ulipoteza cheti chako.

Hati ya polisi inapatikana kutoka kituo chochote cha polisi kilicho karibu nawe.

Ukipoteza au kuharibu cheti chako, unapaswa kuripoti kwa polisi.

5. Nakala za hati zako za utambulisho:

Waombaji walio na umri chini ya miaka 18 watahitaji kuwa na nakala za vyeti vyao vya kuzaliwa, ambavyo vinapaswa kuwasilishwa pamoja na nakala ya Kitambulisho (ID) au pasipoti cha mzazi/mlezi.

Watu wazima (wenye umri zaidi ya miaka 18) watahitaji kuwa na nakala za vitambulisho (ID) za kitaifa au ngeni au Pasipoti.

Jina kwenye hati ya utambulisho lazima liwe sawa na jina lililotumiwa katika mitihani ambayo cheti kilichopotea kilitolewa. 

6. Picha ya pasipoti yenye rangi

Kumbuka: Wale ambao wamebadilisha majina yao kisheria lazima wajumuishe hati za kisheria walizotumia kubadilisha majina yao kama vile cheti cha ndoa kwa wanawake au nakala ya notisi ya Gazeti la Serikali ambapo jina lililobadilishwa linaonekana

Hatua za kutuma ombi la kubadilisha cheti cha KNEC: 

Hatua ya 1: Ingia katika tovuti ya Mfumo wa Taarifa ya Kusimamia Maswali ya KNEC (QMIS)

 Maombi ya kubadilisha vyeti vya masomo hufanywa kupitia tovuti ya mtandaoni ya KNEC, Mfumo wa Taarifa za Kusimamia Maswali (QMIS). Utahitajika kuingia kwa kuingiza jina lako la mtumiaji na nenosiri ikiwa tayari una akaunti. Ikiwa huna akaunti, utahitajika kuunda akaunti ili kutumia tovuti hii. Fuata hatua zilizoorodheshwa hapa chini ili kuunda akaunti. 

QMIS homepage.png

Picha ya ukurasa wa kwanza wa tovuti ya QMIS. 

 

Hatua ya 2: Unda akaunti yako ya mtumiaji ya QMIS.

Bofya kwenye kitufe cha "Jisajili" ili kuunda akaunti mpya. Unatakiwa kutoa maelezo yafuatayo unapofungua akaunti yako:

 1. Jina kamili
 2. Nambari ya simu
 3. Anwani yako ya posta
 4. Cheo/nafasi kama vile Bw. Bi
 5. Anwani yako ya barua pepe.

Baada ya kuingiza maelezo yote hapo juu na kuthibitisha anwani yako ya barua pepe, bofya kwenye kitufe cha "Jisajili". Mfumo wa QMIS utaunda akaunti yako kiotomatiki na kutuma jina lako la mtumiaji na nenosiri kwa anwani yako ya barua pepe.

Tumia barua pepe yako kupata jina lako la mtumiaji na nenosiri na kuingia kwenye tovuti ya QMIS.

QMIS Required Information.png

Picha inayoonyesha maelezo utakayohitajika kujaza unapojiandikisha kwa tovuti ya QMIS.

Hatua ya 3: Jaza fomu ya maombi ya mtandaoni na uambatanishe hati zinazohitajika.

Baada ya kuingia kwenye mfumo wa QMS, bofya sehemu ya "Cheti Kilichopotea" ili kupata fomu ya maombi. Weka nambari yako ya Fahirisi (index number) - kitambulisho cha kipekee kinachotolewa kwa watahiniwa ambao wamejiandikisha kufanya mtihani wa KNEC -, Mtihani (KCPE, KCSE), Mwaka na Msururu (mwezi ulipofanya mtihani) kisha ubofye kitufe cha "Tafuta" kisha mfumo. itathibitisha maelezo yako na kutoa jina lako kamili katika kisanduku cha "Jina".

Ambatisha hati zote zinazohitajika katika sehemu ya viambatisho na ubofye kitufe cha "Wasilisha" ili kutuma ombi lako. 

Online application form.png

Picha ya fomu ya maombi ya mtandaoni. 

Ukishatuma ombi lako, KNEC itathibitisha hati zako na kisha kukutumia nambari ya kipekee ya Paybill na nambari ya akaunti kama ujumbe mfupi (SMS)  kwenye nambari ya simu uliyotumia wakati wa usajili ikionyesha jumla ya kiasi unachofaa kulipa ambacho ni Ksh5,220 ( ikijumuisha ushuru (VAT)).

Lipa kupitia huduma ya kutuma pesa  ya simu ya mkononi, MPESA, na KNEC itaanza kuchakata ombi lako. Cheti cha nakala hutayarishwa katika siku kumi na tano (15) za kazi.

Nitafanya nini ikiwa ombi langu litakataliwa?  

Ombi lako linaweza kukataliwa ikiwa:

 1. Maelezo kama vile jina lako, jina la shule au kituo cha mitihani, nambari ya faharasa (index number) katika ombi lako ni tofauti na ile inayotumika katika mtihani.
 2. Ombi lako halijatimiza au kukidhi mahitaji yote.

Ikiwa ombi lako litakataliwa, unaweza kulituma ombi tena kwa kuondoa ombi la zamani na hati zote zilizoambatishwa kwenye tovuti na kisha kupakia taarifa sahihi na hati zinazotakikana. 

Utapata wapi cheti chako? 

KNEC itakuarifu kupitia maelezo ya mawasiliano uliyotumia kusajili akaunti yako mara tu ombi lako litakaposhughulikiwa na nakala ya cheti kuwa tayari kuchukuliwa katika afisi zao. 

Nenda kwa ofisi ya KNEC mwenyewe ukiwa umebeba kitambulisho chako halali au pasipoti ili kuchukua nakala ya cheti chako.

Waombaji walio chini ya umri wa miaka 18 lazima waambatane na mzazi au mlezi rasmi. Mzazi au mlezi lazima aonyeshe kitambulisho chake halisi na cheti halisi cha kuzaliwa cha mtoto. Unaweza kujifunza zaidi kuhusu jinsi ya kupata cheti cha kuzaliwa katika makala hii. 

Unaweza pia kuangalia hali ya ombi lako kwa kuingia kwenye Mfumo wa Taarifa ya Kusimamia Maswali ya KNEC (QMIS).

Kumbuka: Ikiwa cheti hakitakusanywa baada ya miaka MIWILI (2) kuanzia tarehe ya kutuma ombi, KNEC itaiondoa bila kuwasiliana na mwombaji na haitarejesha pesa zilizolipwa.

Anwani muhimu za mawasiliano na msaada

 1. Afisa Mkuu Mtendaji (CEO) wa KNEC kupitia barua pepe ceo@knec.ac.ke ama  archives@knec.ac.ke
 2. Ofisi Kuu ya Baraza la Kitaifa la Mitihani la Kenya (KNEC) iliyoko  New Mitihani House (NMH) kwenye Barabara ya Popo (Popo Road) iiliyoko eneo la South C, Nairobi. 
 3. Simu: +254 020 3317412 / 3317413 / 3317419 / 3317427 / 3341027 3341050 / 3341071 / 3341098 / 3341113 / 2213381
 4. Nambari ya simu ya mkononi (mobile): 0720741001/0732333860
 5. Bambari ya Faxsi+254-020- 2226032
 6. Anwani ya Barua Pepe (email): exams@knec.ac.ke
 7. Tovuti: https://www.knec.ac.ke/

Ikiwa una maswali yoyote, tafadhali tuandikie kupitia ukurasa wa Facebook wa Julisha.Info au zungumza nasi kupitia WhatsApp (+254110601820) ,Jumatatu hadi Ijumaa kutoka 08:00 asubuhi hadi 5:00 jioni