Kujitia kitanzi kunamaanisha nini?

Kujitia kitanzi ni pale mtu anapojiumiza kimakusudi akiwa na nia ya kukatisha maisha yake, na matokeo yake huwa ni kifo.

Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) linakadiria kuwa kila sekunde 40, mtu mmoja hufa kwa kujiua. Ulimwenguni, kujitia kitanzi ni sababu ya nne inayoongoza ya vifo kati ya vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 29.

Zaidi ya hayo, takwimu kutoka kwa WHO zinaonyesha kuwa watu 6 kati ya 100,000 hufa kwa kujitia kitanzi nchini Kenya.

Ninaweza aje kujua ikiwa mtu yuko katika hatari ya kujitia kitanzi?

Kuna mambo kadhaa ambayo yanaweza kumfanya mtu afikirie, ajaribu, au afe kwa kujiua. Hizi ni pamoja na:

 • Mtu ambaye amejaribu kujitia kitanzi hapo mbeleni ana uwezekano mkubwa wa kufanya hivyo tena.
 • Kupitia vurugu na unyanyasaji kama vile unyanyasaji wa watoto, kudhulumiwa, unyanyasaji wa kijinsia, migogoro na vita kwa kawaida huhusishwa na ongezeko la hatari ya kupata mfadhaiko, wasiwasi na hali zingine ambazo zinaweza kumfanya mtu awe katika hatari kubwa ya kujiua.
 • Magonjwa ya akili kama vile unyogovu na ugonjwa wa kubadilika kwa hisia yanaweza kusababisha mtu kuwa na hisia kali na mchanganyiko, ikiwa ni pamoja na hisia za kukata tamaa, na wanaweza hata kujaribu kujiua.
 • Kuna uwezekano mkuwa wa mtu aliye na mawazo ya kujiua kujaribu kujiua ikiwa anahisi kunyanyapaliwa na kudharauliwa kuhusu kupata msaada na kuzungumza juu ya ugonjwa wa akili.
 • Huzuni, unyanyapaa na dharau, na msongo wa mawazo ni mambo ya kawaida miongoni mwa wale ambao wamefiwa na mpendwa wao kwa kujiua, jambo ambalo huongeza hatari yao ya kuwa na mawazo ya kujiua.
 • Unywaji pombe na matumizi haramu ya dawa za kulevya yanaweza kumfanya mtu kuwa na hisia zilizochanganyika, jambo linaloweza kumfanya awe na  mawazo ya kujiua.
 • Kuwa na magonjwa sugu kama na maumivu ya kudumu kama vile saratani au ugonjwa wa arthritis, ni mzigo mzito kihisia na unaweza kumfanya mtu ajisikie kama hana usemi wowote kuhusu maisha yake. Mtu huyo anaweza kuhisi kuwa ametegwa na kufungiwa, jambo linaloweza kumfanya kuwa na mawazo ya kujitia kitanzi na hata kujaribu kujiua ili kuepuka hisia na hali hiyo.
 • Ikiwa mtu anaweza kupata njia anazoweza kutumia kujiumiza au kujiua
 • Mawazo ya kutaka kujitia kitanzi yanaweza kutokea kwa baadhi ya watu wanapopatwa na matukio fulani ya maisha, kama vile kufiwa na mpendwa, kuhangaika kifedha, kuvunjika moyo au kupewa talaka, kunyanyaswa, au kupata matokeo mabaya  shuleni.

Baadhi ya ishara za onyo la kujitia kitanzi ni zipi?

 • Kuzungumza kuhusu kutaka kufa au kujiua. Kwa mfano, "Natamani ningekufa".
 • Kuzungumza kuhusu kutokuwa na tumaini na kutokuwa na sababu ya kuishi.
 • Kupanga au kutafiti kuhusu njia za kufa au kuchukua maisha yao.
 • Kuzungumza  kuhusu kuwa katika maumivu mengi au kuhisi kunaswa.
 • Kupatiana mali muhimu ya kibinafsi.
 • Kuzungumza kuhusu kuhisi kuwa wao ni mzigo kwa wengine.
 • Mabadiliko yanayoonekana katika tabia kama vile kulala kupita kiasi, kutolala kabisa, kujitenga au kujitenga na familia na marafiki, kuongezeka kwa matumizi ya pombe na dawa za kulevya, mabadiliko makubwa ya hisia, kuwa msukumo au kutojali.
 • Kuaga marafiki na familia kana kwamba hawatakutana tena.

Soma zaidi hapa kuhusu hali zinazoweza kuathiri uwezekano wa mtu kujaribu kujiua na ishara za onyo kutoka kwa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa(CDC)

Dhana za kawaida kuhusu kujitia kitanzi.
Majadiliano kuhusu kujiua ni nadra katika jamii nyingi, huku watu wengi wakiwa na taarifa zisizo sahihi kuhusu jambo hili. Baadhi ya dhana za kawaida kuhusu kujiua ni pamoja na:

SWA_Suicide_Myths_and_Facts__1_.png

Mchoro unaoonyesha baadhi ya dhana na ukweli kuhusu kujitia kitanzi.

Unaweza aje kumsaidia mtu mwenye mawazo ya kujitia kitanzi?
Ikiwa mtu unayemjua anafikiria kujiua au unaona akiwa na dalili zilizotajwa hapo juu, kuwa makini na uzichukulie kwa uzito. Waambie kwamba unajali na kwamba hawako peke yao. Zaidi ya hayo, unaweza kusaidia kuzuia kujiua kwa:

 1. Kuuliza maswali ya moja kwa moja: Jua kama wanafikiria kujitia kitanzi, unaweza kuuliza, "Je, unafikiria kujiumiza/kujiua?", na ikiwa wamefikiria njia watakazotumia kuchukua maisha yao. Hii itakusaidia kujua ikiwa mtu huyo yuko katika hali ya hatari na kupata msaada.
 2. Kuwaweka salama: Unaweza kufanya hivi kwa kumzuia mtu kupata vitu kama vile dawa, kamba, au vitu vyenye ncha kali ambavyo vinaweza kutumika katika kujiua.
 3. Kuwashawishi kutafuta msaada kutoka kwa mtaalamu wa afya ya akili: Wataalamu wa afya ya akili wamefunzwa jinzi ya kuwasaidia watu walio katika dhiki. Ikiwa mpendwa wako anasita kumtembelea mmoja, unaweza kujitolea kuandamana naye kwenye miadi yao.
 4. Onyesha Upendo: Kukaa nao, kuzungumza nao kwa na kuwasikiliza kutawakumbusha kwamba kuna mtu anayewajali.

SWA__Support_for_suicidal_thoughts.png

Mchoro unaoonyesha baadhi ya njia unazoweza kumsaidia mtu mwenye mawazo ya kujitia kitanzi

Mahali pa kupata msaada
Wasiliana na nambari zifuatazo ikiwa una dhiki inayohusiana na afya ya akili au una wasiwasi kuhusu mpendwa ambaye anaweza kuhitaji usaidizi wa afya ya akili.

(Maelezo yaliyo hapa chini yanalenga kuwahudumia wakimbizi katika kambi tofauti nchini Kenya. Tafadhali wasiliana na hospitali iliyo karibu nawe ikiwa hauko katika kambi za wakimbizi.)

1. Kakuma 

SHIRIKANAMBARI YA SIMU
International Rescue Committee (IRC)0792067135
Humanity & Inclusion (HI)0725456334
Danish Refugee Council (DRC)0800720414
Jesuit Refugee Services (JRS)0741417977
Lutheran World Federation (LWF)0800721330
Center for Victims of Torture (CVT) 0759740838

 

2.  Dadaab:

SHIRIKANAMBARI YA SIMU
Kenya Red Cross Society (KRCS)0701494904
International Rescue Committee (IRC)0704600513  
Doctors Without Borders (MSF)0790205727

 

Makala haya yalitayarishwa kwa usaidizi wa Kundi la wataalamu wa Afya ya Akili na Msaada wa Kisaikolojia (MHPSS) katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma.

Ikiwa una maswali yoyote, tafadhali tuandikie kupitia ukurasa wa Facebook wa Julisha.Info au zungumza nasi kupitia WhatsApp (+254110601820), Jumatatu hadi Jumamosi kutoka 08:00 asubuhi hadi 5:00 jioni