Kampeni ya Malezi Bora ni nini?

Malezi Bora ni shughuli maalum inayofanywa mara mbili kila mwaka nchini Kenya ili kuijulisha umma kuhusuafya bora na lishe kwa akina mama na watoto wao. Kipindi cha kampeni hii pia kinajulikana kama wiki za Malezi Bora. Kampeni za Malezi Bora zilianzishwa mwaka 2007 na Wizara ya Afya ya Umma na Usafi wa Mazingira kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF).

Kampeni hii inazingatia:

 • Kuwapa virutubisho vya Vitamini A watoto wote wenye umri kati ya miezi sita na chini ya miaka 5 ili kuongeza kinga yao.
 • Kuwapa tembe za minyoo watoto wote wenye umri kati yam waka mmoja na chini ya miaka 5.
 • Kuwachunguza watoto wote wenye umri kati ya miezi sita na chini ya miaka 5 kwa utapiamlo mkali kwa kutumia mkanda wa Mid-Upper Arm Circumference (MUAC).
 • Utambulisho na rufaa ya kesi zozote za utapiamlo kwa matibabu.

 

Je, kampeni hii inafanywa vipi katika makazi ya Kalobeyei na kambi za wakimbizi za Kakuma na Dadaab (Dagahaley, Ifo, Hagadera)?

Wahudumu wa afya hutembelea nyumba zote katika sehemu hizi ili kuwatafuta watoto wenye umri kati ya miezi sita na chini ya miaka 5.

 • Katika kambi ya Hagadera, kampeni hii huendeshwa na wahudumu wa afya kutoka shirika la International Rescue Committee (IRC).
 • Kule Ifo, wahudumu wa afya kutoka Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya (Kenya Red Cross Society) hufanya kampeni hiyo.
 • Katika kambi ya Dagahaley shirika la Medecins Sans Frontieres (MSF) huongoza kampeni ya Malezi Bora.
 • Huko Kakuma 1, 3 na 4, kampeni ya Malezi Bora huongozwa na wahudumu wa afya kutoka shirika la IRC. Wahudumu wa Afya kutoka Huduma za Afya za Kanisa la African Inland Church (AIC) huongoza kampeni hiyo huko Kakuma 2.
 • Katika makazi ya Kalobeyei, kampeni hiyo inaongozwa na wahudumu wa afya kutoka Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya (Kenya Red Cross Society) na wa Huduma za Afya za Kanisa la African Inland Church (AIC).
 • Wenyeji wa maeneo yanayozunguka kambi ya Hagadera wanaweza kutembelea vituo vya afya vya Borehole 5 na Alinjugur kwa huduma za Malezi Bora.
 • Huko Kakuma, Watoto kutoka jamii ya wenyeji wanaweza kupata huduma za Malezi Bora kutoka kwa vituo vya afya vya umma kama hospitali ya Kaunti Ndogo ya Turkana Magharibi.

Kampeni  hii hufanyika lini?

Kampeni za Malezi Bora hufanyika kila mwaka katika miezi ya Mei na Novemba kote nchini. Katika kipindi hiki, watoto wote wenye umri wa miezi sita hadi miaka mitano hupewa virutubisho vya Vitamini A na tembe ya minyoo.

Nitajua aje wakati maafisa wa afya wanakuja nyumbani kwangu?

Mashirika yote yanayohusika na kampeni za Malezi Bora yataarifu umma kupitia viongozi wa jumuiya na kambi, vituo vya redio, Julisha.Info, mifumo ya matangazo ya umma na kupitia wafanyakazi wa afya walioko kambini.

Nitafanya nini mtoto wangu akikosa kampeni ya Malezi Bora?

Iwapo mtoto wako atakosa kushiriki kampeni ya Malezi Bora, tembelea kituo cha afya kilicho karibu nawe. Wahudumu wa afya watampa mtoto kirutubisho cha Vitamini A na tembe ya minyoo.

Virutubisho vya Vitamini A humsaidiaje mtoto?

Ukosefu wa vitamini A hudhoofisha kinga ya mtoto. Hii ina maana kwamba mwili wa mtoto hautaweza kupambana na maambukizi ya kawaida, na kumweka mtoto katika hatari kubwa ya kupata magonjwa ambayo yanaweza kusababisha kifo.

Vitamini A pia husaidia kuzuia mambo ambayo yanaweza kusababisha upofu kwa mtoto.

irc_worker.png

Mfanyakazi wa Afya wa IRC ampa mtoto kirutubisho cha Vitamini A.

 

 

Vitamin A hutolewa vipi kwa mtoto?

Vitamini A inatolewa kama tone kutoka kwenye kapsuli. Vidonge hivyo vina rangi ya bluu au nyekundu, huku kipimo cha Vitamini A kwenye kidonge cha bluu kikiwa kidogo ikilinganishwa na kipimo cha Vitamini A kwenye kidonge chekundu. Vitamin A kutoka kidonge cha bluu hutolewa kwa watoto wenye umri wa miezi sita hadi 11, na ya vidonge vyekundu hutolewa kwa watoto wenye umri wa kuanzia mwaka mmoja hadi chini ya miaka 5.

supplement.png

Vidonge vyekundu na bluu vya Vitamin A. Picha kwa hisani ya UNICEF

Je, kirutubisho cha Vitamini A ni salama kwa watoto?

Ndio. Vitamini A hulinda watoto dhidi ya magonjwa kama vile kuhara, magonjwa ya kifua, na husaidia kuzuia kifo.

Ili kuhakikisha kuwa watoto wanapata Vitamini A ya kutosha, hakikisha kuwa unawapa vyakula kama spinach, karoti, viazi vitamu, maembe, mayai na maziwa.

Kwa nini watoto hupewa tembe za minyoo?

Wakati wa Malezi Bora, watoto wenye umri wa kati ya mwaka mmoja hadi mitano hupewa tembe za kuua minyoo inayopatikana katika miili wa watoto. Minyoo huchangia ukuaji wa utapiamlo katika miili ya watoto. Kwa kuhakikisha kuwa mtoto wako anapokea tembe ya minyoo, unasaidia kuboresha afya yake kwa ujumla na kuzuia utapiamlo.

Kwa nini  vipimo vya mkono wa mtoto vinachukuliwa?

Upimaji wa upana wa mkono wa mtoto ni zoezi la kawaida ambayo husaidia maafisa wa afya wanaoendesha kampeni ya Malezi Bora kubaini utapiamlo kwa watoto. Hii inafanywa kwa kupata vipimo vya Mid Upper Arm Circumference (MUAC) vya watoto wenye umri wa kati ya miezi sita na chini ya miaka mitano kwa kutumia mkanda wa rangi ambao hufungwa kwenye mkono wa kushoto wa mtoto. Mkanda huo ni chombo maalum kinachotumiwa kuchukua vipimo vya mkono wa mtoto ili kujua hali ya lishe ya mtoto.

muac.png

Vipimo vya MUAC vya mtoto. Masomo wa kijani kwenye mkanda kunamaanisha kuwa mtoto amelishwa vizuri. Picha Kwa Hisani

Je, rangi kwenye mkanda wa MUAC zinamaanisha nini?

Mkanda inayotumika kuchukua vipimo vya MUAC imewekwa alama za rangi ili kuonyesha viwango vya utapiamlo kwa watoto wadogo.

muac_real.png

Mfano wa Mkanda wa MUAC. Picha kwa hisani ya UNICEF

RANGI NYEKUNDU inamaanisha kuwa mtoto ana utapiamlo mkali na anafaa kupelekwa hospitali kwa matibabu mara moja.

RANGI YA MANJANO inamaanisha kuwa mtoto ana utapiamlo wa wastani na anapaswa kupelekwa hospitali kwa ajili ya virutubisho vya lishe kama vile plumpy sup.

RANGI YA KIJANI inamaanisha kuwa mtoto amelishwa vizuri.

 

swa_kids.png

Dalili za kawaida za utapiamlo kwa watoto.

Watoto wenye utapiamlo husaidiwa kwa njia gani?

 • Watoto wenye utapiamlo mkali au wa wastani hupokea matibabu yanayolingana na mahitaji yao ya lishe na ya kiafya. Watoto hao hutambuliwa kutoka kwa jamii na kuanza kutibiwa kwa utapiamlo
 • Katika kambi ya Dadaab, watoto wengi walio na utapiamlo mkali na utapiamlo wa wastani hupata matibabu manyumbani mwao kwa kutumia vyakula vya tiba vilivyo tayari kutumika vijulikanavyo kama RUTF na matibabu ya kawaida ya hospitali. RUTF hutengenezwa kwa kutumia siagi ya njugu, maziwa, sukari, mafuta ya mboga, madini na vitamini.
 • Huko Kakuma watoto wenye utapiamlo mkali hupewa tiba ya vyakula vya RUTF, huku watoto wenye utapiamlo wa wastani wakipewa vyakula vya nyongeza vilivyo tayari kutumika vijulikanavyo kama RUSF ili kuongeza chakula wanachotumia kila siku.
 • Vyakula vya RUTF na RUSF zina nguvu nyingi na protini ili kumsaidia mtoto mwenye utapiamlo kupona na kuongeza kilo. Virutubisho hivi vinapaswa kutumika vile vilivyo bila kupikwa, kuchanganywa au kuongezwa maji.
 • Panapo haja, watoto walio na utapiamlo mkali ambao pia wana matatizo ya kiafya au kukosa hamu ya kula hulazwa hospitalini kwa matibabu zaidi.


plumpy.png

Plumpy Sup na Plump nut, mifano ya virutubisho vya RUSF na RUTF ambavyo hutolewa kwa watoto walio na utapiamlo.

Je, una maswali yoyote kuhusu kampeni ya Malezi Bora? Tuandikie ujumbe mfupi kupitia ukurasa wetu wa Facebook Jumatatu hadi Ijumaa kutoka 08:00 asubuhi hadi 5:00 jioni.