Marriage.jpg

Kuna matukio maishani, kama vile wakati wa kuomba visa, pasipoti, au kibali cha kufanya kazi, au wakati wa kusajili akaunti ya pamoja ya benki, ambapo kama mkimbizi nchini Kenya, utahitajika kudhibitisha kuwa wewe na mwenzako mmeoana kisheria. Kwa hivyo ni muhimu kuwa na hati inayodhibitisha muungano huo mara tu unapo oa ama kuolewa.

 

Nakala hii itakuonyesha mahitaji ya kufunga ndoa nchini Kenya.

 

Sheria ya Ndoa (2014) inatambua mifumo ifuatayo ya ndoa:

 • Ndoa za Kisheria
 • Ndoa za Kikristo
 • Ndoa za Kihindu
 • Ndoa za kimila
 • Ndoa za Kiislamu

Unahitaji nini kusajili ndoa?

Ili kuoa ama kuolewa nchini Kenya, utahitaji:  

 • Kuwa na umri wa miaka 18 na zaidi
 • Kuwa katika uhusiano na mtu wa jinsia tofauti
 • Usiwe umeolewa ama kwenye uhusiano wa kisheria na mtu mwingine
 • Kuwa na uwezo wa kuelewa maana ya ndoa na kukubaliana nayo (ridhaa)

Ndoa za Kisheria, Kikristo na Kihindu

Ili kufunga ndoa za Kisheria, Kikristo au Kihindu, utahitaji kuandika barua rasmi (ilani) siku zisizopungua 21 kabla ya siku mnayopanga kufunga ndoa kwa Msajili wa Ndoa.

Wewe na mchumba wako mnatakiwa kufika kwa Msajili wa ndoa ili kujaza fomu ya ilani na kushikamana na hati zifuatazo:

 • Kitambulisho cha Mkimbizi au hati ya kusubiri (Nakala na asili)
 • Picha moja ya ukubwa wa pasipoti kwa kila mwombaji
 • Nakala ya Cheti cha Kifo (ikiwa mwombaji ni mjane)
 • Nakala ya Amri ya Talaka (Ikiwa mwombaji alikuwa ameoa hapo awali)
 • Hati ya kiapo ya kudhibitisha hali ya ndoa iwapo Amri ya Talaka au Cheti cha Kifo kina zaidi ya miaka 2.
 • Nakala ya leseni ya mfungaji ndoa (mtu aliyesajiliwa kufunga ndoa)
 • Namba tambulishi (serial number) ya kitabu cha ndoa kitakachotumiwa (inapatikana kutoka kwa mtu atakayewaunganisha katika ndoa)
 • Kadi ya mwaliko wa harusi

Wakimbizi ambao hawana kitambulisho cha wakimbizi au hati ya kusubiri lakini wangependa kusajili ndoa zao wanaweza kutumia Dhibitisho la Usajili (Manifest).

Wanandoa lazima wawe wamefikia umri halali wa ndoa [miaka 18] ili ndoa ifanyike. Ndoa lazima ifungwe ndani ya siku 90 baada ya ilani ya kufunga ndoa kutolewa.

Baada ya muda huo wa ilani ya siku 21 kupita na ndoa hiyo kutopingwa, mtatakiwa kuchukua kiapo kama mtakavyoongozwa na Msajili wa Ndoa ambaye pia huapisha kiapo hicho na kujaza fomu ya Cheti cha Ndoa.

Ukiwa Kakuma, unaweza kutembelea ofisi ya Msajili Msaidizi wa Ndoa huko Lodwar katika ofisi ya Kamishna wa Kaunti ya Turkana. Huduma za usajili wa ndoa zinapatikana pia huko Daadab katika ofisi ya Kamishna wa Kaunti ya Garissa na kwenye ghorofa ya chini ya Sheria House inayopatikana kwenye barabara ya Harambee, mjini Nairobi.

 

Usajili wa ndoa unagharimu shillingi ngapi?

Utahitajika kulipa Ksh 600 ili kujaza fomu ya ilani/notisi ya ndoa.  

Baada ya muda huo wa ilani ya siku 21 kupita na ndoa hiyo kutopingwa, mtatakiwa kuenda kwa msajili wa ndoa kwa mahojiano na kuthibitisha hati zenu.

 • Ksh 600 kujaza Notisi ya Ndoa katika ofisi ya Msajili wa Ndoa.
 • Lipa Ksh 2700 baada ya kipindi cha notisi ya siku 21. Ada hii inahudumia hati ya kiapo, cheti cha ndoa na sherehe ya kufunga ndoa. Itatumika ifuatavyo:

- Sherehe ya Ndoa - Kshs.2000

- Cheti cha Ndoa - Kshs.500

- Kuagiza - Kshs.200

Kwa ndoa za kisheria zinazofungwa na Msajili wa Ndoa nje ya ofisi yake, waombaji watatakiwa kulipa ada zaidi ya Ksh 16,500.

Ndoa ya Kiislamu

Ndoa kati ya wakimbizi wa imani ya Kiislamu inasimamiwa na Kadhi Mkuu au Sheikh / Imam aliyeidhinishwa na Msajili wa Ndoa.

Baada ya hayo, Kadhi atatoa maelezo ya ndoa kwa Msajili kwa Ndoa.

Masharti ya kufunga ndoa

Islamic_Marriage.png

 • Idhini - Bwana harusi na bibi harusi lazima wakubaliane kufunga ndoa, kwa maneno na kwa maandishi. Hii inafanywa kupitia pendekezo rasmi la ndoa (Ijab) na kukubali pendekezo (Qabul).
 • Mahr – Hii inajulikana ama mahari ama zawadi ya bibi harusi.
 • Mashahidi - Mashahidi wawili wenye umri zaidi ya miaka 18 wanatakiwa kuthibitisha mkataba wa ndoa.
 • Wanandoa wanatakiwa kuwa na umri zaidi ya miaka 18.
 • Wanandoa wanapaswa kuwa na akili timamu.
 • Wali - mlezi wa kiume ambaye anaangalia masilahi ya bi harusi.

Wali lazima awepo kwenye sherehe ya ndoa (Nikah) na jina lake, nambari ya kitambulisho chake na saini yake itaonekana kwenye cheti cha ndoa. Hata hivyo, bibi harusi lazima pia aeleze nia yake ya kuingia kwenye ndoa. Idhini haiwezi kutolewa na wale ambao kisheria hawawezi kuitoa kama watoto, watu ambao wana upungufu, au wale walio na ulemavu wa akili ambao hupunguza uwezo wao wa kuelewa idhini.

Usajili wa ndoa unagharimu shillingi ngapi?

 • Ksh 1,000 kwa cheti cha ndoa.
 • Ksh 1,000 kwa mchakato wa kuomba kufunga ndoa
 • Ksh 3,000 kwa sherehe ya kufungwa kwa ndoa (Nikah).
 • Ksh 3,500 kwa kufungwa kwa ndoa (Nikah) kati ya mkimbizi na mtu asiyekuwa mkimbizi

Mkimbizi pia anaweza kupata cheti cha ndoa hata ikiwa hakufunga ndoa kaika korti ya Kadhi. Hii inamaanisha kuwa ikiwa ndoa yako ilifanyika kulingana na tamaduni za Kiislamu lakini hakukuwa na Kadhi, korti ya Kadhi inaweza kukusaidia kupata cheti cha ndoa mara tu Kadhi atakaporidhika kuwa ndoa hiyo ilifanywa kihalali.

 Baada ya kufunga ndoa, cheti cha ndoa kinatolewa ndani ya siku moja.

 

Je, kuna masharti mengine haswa kwa wakimbizi?

Wanandoa wanapaswa kuwa na kitambulisho cha Mkimbizi au hati ya kusubiri (Mandate)

Wanandoa hawapaswi kuwa jamaa.

Je, unatafuta ushauri na usaidizi wa kisheria bila malipo katika kusajili ndoa au talaka? Unaweza kuwasiliana na shirika la Kituo Cha Sheria kwa usaidizi. 

Kituo Cha Sheria ni shirika la usaidizi wa kisheria nchini Kenya ambalo hutoa huduma za kisheria bila malipo kwa wale ambao hawawezi kumudu. Shirika hilo lina afisi Nairobi, Mombasa, na afisi ya tawi katika eneo la Pangani, Nairobi, kutoa usaidizi wa kisheria kwa watu binafsi na jamii kote nchini. 

Ofisi kuu 

Ofisi kuu ya Kituo Cha Sheria iko kwenye makutano ya barabara ya Ole Odume na barabara ya Argwings Kodhek, mkabala na tume kuu ya Bangladesh. Unaweza kuwasiliana na makao makuu kwa kupiga simu 0734 874221 au 0727 773991 au kwa barua pepe info@kituochasheria.or.ke 

Ofisi ya Mombasa 

Kwa wale wanaoishi Mombasa, Kituo cha Ofisi ya Mkoa wa Pwani iko kwenye Mtaa wa Taratibu huko Tudor, karibu na chuo kikuu cha kiufundi cha Mombasa na karibu na Hoteli ya White Rhino. Unaweza kufikia timu kwa kupiga simu 0731 129739 au 0700 638379, au kwa barua pepe msa@kituochasheria.or.ke 

Ofisi ya Pangani 

Kituo Cha Sheria pia wana ofisi ya tawi katika eneo la Pangani la Nairobi, iliyoko KCDF House, ghorofa ya 4, Barabara ya Chai/Pamba, nje ya Barabara ya Juja. Ofisi ya tawi ya Pangani inaweza kupatikana kwa kupiga simu 0736 867241 au 0720 806531, au kwa barua pepe fmp@kituochasheria.or.ke 

Unaweza pia kutuma hoja yako ya kisheria kama ujumbe mfupi wa maandishi kwa Kiingereza au Kiswahili kwa 0700777333 na usubiri jibu kutoka kwa wataalamu wa sheria wa Kituo.

 

Iwapo una maswali yoyote, wasiliana nasi kupitia ukurasa wa Julisha.Info wa mtandao wa Facebook, kila Jumatatu hadi Jumamosi kutoka saa 2 asubuhi hadi saa 11 jioni.