Lutta Blood donation.JPG

Mhudumu wa afya wa IRC atoa damu wakati wa waku ya wanaotoa damu ulimwenguni 2023

Utoaji wa damu ni mchakato wa hiari ambayo mtu anatoa damu yake kwa mtu mwingine, mara nyingi mgonjwa ambaye anahitaji damu kwa ajili ya matibabu. Daktari lazima aamue ni nani anayehitaji damu na ni nani anayeweza kutoa damu. Kupitia utaratibu rahisi, mtu anaweza kutoa damu yote au kutoa sehemu maalum za damu yake kama vile pleteleti za damu (platelets), seli nyekundu za damu (Red blood cells), au plasma, ingawa aina ya kawaida ni ya kutoa damu yote kwa jumla.

Damu iliyotolewa ni muhimu kwa taratibu mbalimbali za kuokoa maisha, ikiwa ni pamoja na upasuaji, matibabu ya ajali, matibabu ya saratani, matatizo wakati wa kujifungua, na kudhibiti magonjwa ya damu kama vile upungufu wa damu na hemofilia. Damu haiwezi kutengenezwa kwingine ila mwilini. Damu ina tarehe ya mwisho wa matumizi (siku 21-35) na mahitaji ya mara kwa mara hutegemea utoaji wa hiari. Kwa kutoa damu, unachangia moja kwa moja kuhakikisha upatikanaji wa damu kwa wale wanaohitaji, hivyo kuokoa maisha mengi.

Katika makala haya, tutaangalia mchakato wa kutoa damu yote (whole blood) na kutoa maelezo juu ya maswali kadhaa ambayo unaweza kuwa nayo.

Mchakato wa Kutoa Damu

  1. Usajili: Unahitaji kujaza fomu rahisi ya usajili ambayo ina taarifa zote za mawasiliano zinazohitajika kuanza mchakato wa kutoa damu. Hii kawaida huwa katika kituo chochote cha utoaji damu.
  2. Uchunguzi: Tone la damu kutoka kwenye kidole chako litachukuliwa kwa ajili ya kipimo rahisi ili kuhakikisha kwamba kiwango cha chuma (iron) kwenye damu yako kinatosha kwa utoaji damu.
  3. Utoaji: Baada ya kufaulu uchunguzi, utaelekezwa kwenye kitanda cha mtoaji damu kwa ajili ya utoaji. Hii inachukua kati ya dakika 6-10 tu.
  4. Vinywaji: Unaweza kukaa katika eneo la kusubiri hadi ujisikie mwenye nguvu ya kutosha kuondoka kituoni. Katika hali nyingi, timu zinazofanya kampeni za utoaji damu zinatoa vinywaji kwenye eneo la utoaji damu. Hii husaidia kuwaepusha wachangiaji damu kupata kizunguzungu au matatizo mengine kutokana na kiwango cha chini cha sukari.
  5. Vipimo: Damu inachunguzwa kwa virusi vya HIV, Hepatitis A & B pamoja na maambukizi mengine.
  6. Ukusanyaji wa Matokeo: Unaweza kuchukua matokeo yako katika kituo ambacho ulitoa damu.

Vigezo vya kustahiki vya kutoa damu nchini Kenya

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Tishu na Upandikizaji ya Kenya, ili kutoa damu, unapaswa kuwa na vigezo vifuatavyo:

  • Umri kati ya miaka 16 na 64.
  • Uzito wa angalau kilo 50 kwa wanawake na angalau kilo 55 kwa wanaume.
  • Asiwe anatumia dawa yoyote.
  • Asiwe amepata chanjo hivi karibuni.
  • Wanawake hawaruhusiwi kutoa damu wakati wa hedhi.
  • Wanawake wanaonyonyesha na wajawazito hawaruhusiwi kutoa damu.
  • Awe katika afya njema wakati wa utoaji damu. Hupaswi kuwa na au kuwa kwenye matibabu ya ugonjwa sugu au ugonjwa wa muda mrefu unaodhoofisha mwili. Watu wenye hali kama vile shinikizo la damu (hypertension), kisukari (diabetes), pumu (asthma), na ugonjwa wa moyo(heart disease) hawaruhusiwi kutoa damu kwani hii inaweza kudhoofisha zaidi uwezo wa mwili wao kushughulikia magonjwa.
  • Aweze kupita uchunguzi wa kimwili na historia ya afya inayofanywa kabla ya utoaji damu. Hii inajumuisha mapitio ya historia yako ya matibabu, viashiria vya afya kama vile shinikizo la damu, joto la mwili, na mpigo wa moyo, ujauzito, umri, na uzito. Uchunguzi huu ni BURE.
  • Asiwe na historia ya hivi karibuni ya kupokea damu au kufanyiwa upasuaji.
  • Wanaume wanaweza kutoa damu tena angalau miezi mitatu baada ya utoaji wao wa mwisho.
  • Wanawake wanaweza kutoa damu tena angalau miezi minne baada ya utoaji wao wa mwisho.

Mambo unayopaswa kufanya siku ya kutoa damu:

  • Kunywa maji mengi (au kinywaji kingine kisicho na pombe) kabla ya kwenda kutoa damu.
  • Kula mlo wenye afya, kuepuka vyakula vyenye mafuta kama chipsi au barafu.
  • Vaa shati lenye mikono ambayo unaweza kukunja juu ya viwiko vya mikono yako.
  • Mwambie daktari kama unayo mkono unaoupenda au mshipa maalum ambao umefanikiwa kutumika kutoa damu hapo awali.
  • Pumzika, sikiliza muziki, zungumza na watoa damu wengine au soma wakati unapotoa damu.

Baada ya kutoa damu:

  • Weka bandeji kwa masaa kadhaa zijazo; ili kuepuka upele wa ngozi, safisha eneo linalozunguka bandeji kwa sabuni na maji.
  • Usifanye kazi nzito au mazoezi makali kwa siku nzima.
  • Ikiwa eneo la sindano linaanza kutoa damu, tumia shinikizo na inua mkono wako moja kwa moja juu kwa dakika 5-10 au hadi damu ikome.
  • Ukipata kizunguzungu au kuhisi kama unaenda kuzimia, acha unachokifanya na ukae chini au lala hadi uhisi vizuri; epuka kufanya shughuli yoyote ambapo kuzimia kunaweza kusababisha jeraha kwa angalau masaa 24.
  • Endelea kula mlo wenye lishe bora hasa ulio na madini ya iron kwa wingi.

Faida za kutoa damu kwa yule anayetoa

Kutoa damu kuna faida kadhaa, kwa yule anayetoa damu na kwa wale wanaopokea damu. Hapa kuna faida muhimu kwa yule anayetoa:

  1. Kujua Kundi la Damu: Unapata kujua aina ya damu yako (A, B, AB au O) na RH Factor yako (Positive au Negative).
  2. Kuboresha Uzaliano wa Damu Mwilini: Baada ya kuchangia damu, mwili unajenga upya seli za damu zilizokosekana. Hii inakuza uundaji wa seli mpya za damu (Seli nyekundu na nyeupe) ambazo zinaimarisha ustawi wako kwa ujumla kwa kusaidia kudumisha idadi ya seli za damu zilizo na afya.
  3. Uchunguzi wa Afya Bila Malipo: Kabla ya kuruhusiwa kuchangia damu, utapitia uchunguzi wa haraka wa kimatibabu kuhakikisha uko sawa kuchangia. Hii inaweza kujumuisha kuangalia shinikizo la damu, viwango vya hemoglobini, uzito, na kundi la damu. Hii inaweza kusaidia kugundua dalili za matatizo ya afya yanayoweza kutokea.
  4. Kuchangia damu ni shughuli ya heshima ambayo ni njia yenye athari ya kuleta tofauti katika jamii yako huku watu wakija pamoja kusaidia wale wanaohitaji. Kumbuka, mchango wako mmoja una uwezo wa kugusa maisha mengi na kuchangia sana katika kujenga jamii yenye afya na nguvu.

*Ni muhimu kutambua kuwa ni wale tu walio na afya njema wanaoweza kuchangia damu. Tafadhali wasiliana na daktari ili kutathmini hali yako ya afya kabla ya kuchangia damu.

Baadhi ya dhana potofu za kawaida kuhusu kuchangia damu

Dhana potovu: Kuchangia damu kunaumiza.

Ukweli: Sindano inayotumika wakati wa kuchangia damu ni sawa na ile inayotumika kwenye kipimo cha kawaida cha damu na watu wengi huivumilia vizuri.

Dhana potovu: Kuchangia damu huchukua muda mrefu.

Ukweli: Kuchangia damu kwa kawaida huchukua takriban dakika 10-15. Ukijumuisha usajili, uchunguzi wa haraka wa kimatibabu, na muda wa kupona, mchakato mzima kwa kawaida huchukua takriban dakika 30.

Dhana potovu: Unaweza kupata magonjwa kutoka kwa kuchangia damu.

Ukweli: Kuchangia damu kunahusisha matumizi ya vifaa salama na vya kutupa, vikifuatwa na taratibu kali za usalama ili kupunguza usumbufu na kuhakikisha uzoefu salama.

Dhana potovu: Kuchangia damu kunaweza kudhoofisha mfumo wako wa kinga.

Ukweli: Kuchangia damu hakuathiri mfumo wako wa kinga. Mwili unachukua nafasi ya damu iliyotolewa haraka.

Dhana potovu: Ni watu wenye aina za damu nadra tu wanaopaswa kuchangia.

Ukweli: Aina zote za damu zinahitajika na ni muhimu. Mabenki ya damu yanahitaji usambazaji wa mara kwa mara wa aina zote za damu ili kukidhi mahitaji ya wagonjwa tofauti.

Dhana potovu: Kuchangia damu kutakufanya uhisi uchovu au dhaifu.

Ukweli: Wachangiaji wengi wanajisikia sawa baada ya kuchangia damu. Baadhi wanaweza kuhisi uchovu kidogo au kizunguzungu, lakini kupumzika na kunywa vinywaji vingi kunaweza kusaidia. Mwili unachukua nafasi ya damu iliyopotea ndani ya siku moja. Inashauriwa kutokujisukuma sana wakati huu.

Dhana potovu: Hauwezi kuchangia damu ikiwa una tattoo au vipini mwilini.

Ukweli: Unaweza kuchangia damu ikiwa una tattoo au vipini mwilini. Hakikisha unasubiri miezi 12 baada ya kupata tattoo kabla ya kutoa damu ili kuhakikisha hakuna hatari ya maambukizi.

 

Ninaweza kutoa damu wapi?

Unaweza kuchangia damu katika mojawapo ya vituo vya mikoa vya Mamlaka ya Uhamisho na Upandikizaji Tishu ya Kenya (KTTA) au vituo vya satelaiti, hapa. Ikiwa uko Kakuma, Hagadera, IFO, na Dagahaley, unaweza kuchangia damu katika maeneo mbalimbali yakiwemo:

 

Eneo

Hospitalinambari za simu

Kakuma

Hospitali ya Amussait 

Hospitali Kuu ya IRC-Kaapoka

0712840234

0110944509

HagaderaHospitali Kuu ya IRC0724268551
IfoHospitali ya KCRS- IFO 10792553906
DagahaleyHospitali ya MSF ya Dagahaley 0113906855

Ikiwa una maswali yoyote, tafadhali tuandikie kupitia ukurasa wa Facebook wa Julisha.Info au zungumza nasi kupitia WhatsApp (+254110601820) ,Jumatatu hadi Ijumaa kutoka 08:00 asubuhi hadi 5:00 jioni