Makala haya yatachunguza Surua(Measles) kama ugonjwa, nini huisababisha, jinsi ya kuambukizwa, ishara na dalili zake, watu walio katika hatari ya kuambukizwa surua, kinga yake na matibabu yake.

Ukambi/Surua ni nini?

Surua ni ugonjwa unaoambukiza sana unaosababishwa na kirusi kiitwacho Morbillivirus ambacho huathiri zaidi mfumo wa upumuaji. Huenea kwa urahisi wakati mtu aliyeambukizwa anapumua, kukohoa, au kupiga chafya nje ya hewa iliyoambukizwa ambayo inapumuliwa na mtu mwenye afya. Surua pia inaweza kuenea kwa kugusana na nyuso au vitu vilivyochafuliwa.

Mara baada ya kuambukizwa, surua inaweza kusababisha ugonjwa mbaya, matatizo mengine na hata kifo. Surua inaweza kuathiri mtu yeyote, lakini ni kawaida kwa watoto. Kupata chanjo ya surua ndiyo njia bora zaidi ya kuzuia maambukizi ya surua na kuenea kwake.

Je, surua huenezwa aje?

Ukambi/Surua ni moja ya magonjwa yanayo ambukiza zaidi duniani. Virusi hubakia hai na huambukiza hewani au kwenye nyuso zilizoambukizwa kwa hadi saa 2 baada ya mtu aliyeambukizwa kuzungumza, kukohoa au kupiga chafya.Mtu mwenye afya njema anapopumua chembechembe kutoka kwa mtu aliyeambukizwa, anaweza kupata virusi vya surua na kisha kuanza kuonyesha dalili za maambukizi. Ni muhimu kutambua kwamba mtu 1 aliyeambukizwa anaweza kuambukiza angalau watu 9 kati ya 10 ambao hawajachanjwa.

Je dalili na ishara za Surua ni kama zipi?

Ishara na dalili za surua huanza kuonekana siku 10-14 baada ya kuambukizwa virusi. Upele kwa kawaida ni dalili inayoonekana zaidi ya surua. Dalili za mapema kawaida huchukua siku 4-7. Zikiwa ni pamoja na:

  • Kutokwa kwa makamasi mengi puani
  • Kikohozi
  • Macho mekundu na yenye maji
  • Madoa meupe madogo ndani ya mashavu

Takriban siku 7-18 baada ya kuambukizwa, unaweza kuanza kuona upele. kwa kawaida kwenye uso na shingo ya juu ambapo huenea kwa muda wa siku 3, hatimaye kwenye mikono na miguu. Inaweza kudumu siku 5-6 kabla ya kufifia Mtu anaweza pia kuanza kuumwa na koo, madoa meupe mdomoni, maumivu kwenye misuli na kuhisi mwanga zaidi.

Screenshot 2024-06-04 120512.png

Mtoto mwenye vipele kutoka kwa surua. Picha kwa hisani ya WHO.

Matatizo ya surua yanaweza kusababisha kifo. Baadhi ya matatizo haya ni pamoja na:

  • Upofu
  •  Encephalitis (maambukizi ambayo husababisha uvimbe wa ubongo na uharibifu unaowezekana wa ubongo)
  • Kuharisha sana na upungufu wa maji mwilini (kupungua kwa maji mwilini)
  • Maambukizi ya sikio
  • Matatizo makali ya kupumua ikiwa ni pamoja na nimonia

Matatizo haya yanapatikana zaidi katika:

  • Wanawake wajawazito; Ikiwa mama mjamzito atashika surua wakati wa ujauzito, inaweza kuwa hatari kwake na wakati mwingine inaweza kusababisha mtoto wake kuzaliwa kabla ya wakati na uzito mdogo.
  • Watoto chini ya miaka 5; Hasa kwa watoto walio na kinga dhaifu, kwa mfano wale walio na utapiamlo, wasio na vitamini A ya kutosha au wale walio na virusi vya ukimwi au magonjwa mengine. Surua pia hudhoofisha kinga ya mwili na kuuacha mwili kuwa shabaha rahisi ya maambukizo mengine.
  • Watu wazima zaidi ya miaka 30; Ingawa watu wazima hawako katika hatari zaidi ya surua, wana uwezekano wa kupata matatizo makubwa zaidi ikiwa watapata maambukizi ya surua.

Ni nani aliye katika hatari zaidi ya kuambukizwa surua?

  • Watu wasio na kinga, hawa ni pamoja na wale ambao hawajachanjwa na watu ambao hawakupata kinga baada ya chanjo.
  • Watoto wadogo ambao hawajachanjwa na wale walio na utapiamlo au kinga dhaifu.
  • Wanawake wajawazito wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata matatizo makubwa ya surua iwapo wameambukizwa.

swahili.png

Je, surua ina tiba?

Hakuna matibabu maalum ya surua. Matibabu kwa kawaida hulenga kupunguza dalili, kumfanya mtu astarehe na kuzuia matatizo. Inashauriwa kula lishe bora na kunywa maji ya kutosha kuchukua nafasi ya maji yaliyopotea kwa kuhara, kutapika au kutokwa na jasho kwa sababu ya homa.

Unawezaje kuzuia surua?

Chanjo ni njia bora zaidi ya kuzuia surua. Watoto wote wanapaswa kupewa chanjo dhidi yake.

Ninaweza kupata wapi chanjo ya surua?

Nchini Kenya, chanjo ya Surua Rubella (MR) inatolewa kama sehemu ya mpango wa kawaida wa chanjo ya watoto. Dozi ya kwanza hutolewa wakati mtoto ana miezi 9 na dozi ya pili inatolewa akiwa na miezi 18. Chanjo hii inatolewa bure katika vituo vyote vya afya vya serikali nchini kote.

Unaweza kupata chanjo katika Hospitali kuu ya IRC, na vituo vya Afya E6 na L6 huko Hagadera, na vituo vyote vya IRC huko Kakuma.

Ikiwa una maswali yoyote, tafadhali tuandikie kupitia ukurasa wa Facebook wa Julisha.Info au zungumza nasi kupitia WhatsApp (+254110601820) ,Jumatatu hadi Ijumaa kutoka 08:00 asubuhi hadi 5:00 jioni