Je, unatazamia kuunda kikundi kilichofana cha kujisaidia nchini Kenya? Kwanza, unahitaji kuwa na taarifa za kanuni za uendeshaji wa vikundi hivi, kujua aina za vikundi unavyoweza kuunda na mwongozo wa kuandika katiba ya kikundi chako.

Soma nakala hii ili kuelewa mahitaji na manufaa ya kusajili kikundi cha kujisaidia nchini Kenya. Maelezo haya pia yanaweza kuwa vidokezo muhimu kwa wanachama wa kikundi ulicho ndani kwa sasa na marafiki zako ambao wanataka kuanzisha au kupata thamani zaidi kutoka kwa kikundi chao.

Kikundi cha kujisaidia ni nini?

Kikundi cha Kujisaidia (SHG) kinaundwa wakati kikundi cha watu wenye asili sawa ya kijamii na kiuchumi wanapokutana ili kuunda fursa na kuboresha viwango vyao vya maisha. Kikundi cha kujisaidia kinaweza kusaidia wanachama wake kupata ujuzi, mali kwa ajili ya jamii kama vile shule, vituo vya afya na barabara, na kutengeneza fursa za kuwaingizia kipato wanachama. Vikundi vinaweza kujihusisha na biashara kama vile kuuza mboga, kusuka, kushona nguo, kuendesha maduka ya rejareja na miradi ya ufugaji kama vile ufugaji wa kuku na wanyama.

Je, ni sifa zipi za kawaida za vikundi vya kujisaidia nchini Kenya?

 1. Kujiunga na kikundi cha kujisaidia ni kwa hiari na BURE.
 2. Unashiriki katika shughuli za kuzalisha mapato na kupokea mikopo kutoka kwa kikundi kama mwanachama..  
 3. Vikundi huwa na malengo ambayo yanahusiana na mahitaji ya wanachama na yanajulikana na kukubaliwa na wanachama wote.
 4. Wanachama wa kikundi huandaa miongozo ya jinsi ya kuendesha na kusimamia kikundi chao.
 5. Maamuzi ya vikundi ni ya kidemokrasia - Viongozi wa kikundi (Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu, Makamu Katibu na Mweka Hazina) huchaguliwa  na wanachama.
 6. Wanachama wa kukundi huwa na majukumu ya wazi na huchangia kwa kugawana rasilimali zao kwenye kikundi.

Aina za vikundi vya kujisaidia unazoweza kusajili nchini Kenya

Wanachama wa vikundi vya kujisaida kwa kawaida hutoka katika malezi sawa ka kijamii na kiuchumi. Wanachama hujiunga kukusanya rasilimali na kusaidiana. Wanachama wote wa vikundi vya kujisaidia wanahitaji kushiriki katika dhamira, maono, na malengo ya kikundi ili kuhakikisha kuwa kikundi kinafikia malengo yanayotarajiwa. Hii inafanya iwe rahisi kwa kikundi kufikia malengo inayotaka.

Nchini Kenya, unaweza kusajili aina kadhaa za vikundi vya kujisaidia kama vile:

 • Vikundi vya Vijana 
 • Vikundi vya wanawake 
 • Vikundi vya wanaume 
 • Vikundi mchanganyiko (wanachama wake ni wanawake na wanaume)
 • Vikundi vya watu wenye ulemavu
 • Vikundi vya wazee 
 • Vikundi vya Miradi ya Jamii
 • Vikundi Jumuishi vya Wakimbizi 

Kuna umuhimu gani wa kusajili kikundi cha kusaidia?

Kuna faida nyingi za kusajili vikundi vya kujisaidia. Hii ni pamoja na:

 • Kikundi kitapata hadhi ya kisheria ya kufanya kazi nchini Kenya. 
 • Kikundi hicho kinaweza kumiliki mali kwa niaba ya wanachama wake. 
 • Kujisajili husaidia vikundi kukidhi mahitaji ya kufungua na kuendesha akaunti ya benki kwa jina la kikundi. 
 • Usajili husaidia vikundi kupata huduma za mikopo kama vile mikopo kutoka kwa benki na taasisi ndogo za fedha.  
 • Wanachama wa kikundi huwajibika kwa maamuzi ya kifedha ya kikundi.  

Masharti ya kusajili kikundi cha kujisaidia nchini Kenya

Ili serikali ya Kenya isajili kikundi cha kujisaidia, lazima itimize mahitaji haya:

 1. Kuwa na angalau watu kumi (wenye umri wa miaka 18 na zaidi) ambao wanashiriki kikamilifu katika shughuli za kikundi.
 2. Wanachama wanapaswa kuwa na sababu ya pamoja ya kuanzisha kikundi.
 3. Wanachama wote lazima washiriki katika mafunzo ya kabla kujiandikisha  yanayofanywa na Ofisi ya Maendeleo ya Jamii (SDO) katika ngazi ya Kaunti Ndogo.
 4. Kuwa na katiba iliyoandaliwa na wanachama wa kikundi..
 5. Jina la kikundi, dhamira yake, malengo na madhumuni yake yanapaswa kuwa katika katiba ya kikundi.
 6. Fanya uchaguzi wa viongozi wa kikundi.
 7. Kuwa na kumbukumbu za mkutano ambao wanachama wa kikundi walikubali kusajili kikundi hicho.
 8. Kuwa na orodha ya wanachama wote wa kikundi, iliyotiwa saini, na inayoonyesha majina yao / nafasi / Hati ya Utambulisho (Kitambulisho) na saini zao.
 9. Kitambulisho kinachohitajika kwa wakimbizi ni nambari yao ya Kitambulisho cha Mkimbizi (Alien/Refugee ID).
 10. Nakala za vitambulisho vya wanachama (Kitambulisho cha Mkimbizi).
 11. Lipa ada ya usajili wa kikundi ya KES 1,000/-katika ofisi ya usajili.

Kwa makundi ya wakimbizi, utahitaji pia:

 • Ripoti ya mafunzo ya kikundi kutoka Kurugenzi ya Maendeleo ya Jamii
 • Ripoti ya uthibitishaji kutoka kwa Idara ya Huduma kwa Wakimbizi (DRS). Ripoti hii inatolewa kwa kikundi baada ya DRS kufanya ukaguzi wa wanachama wa kikundi kuhakikisha kuwa ni wakimbizi waliosajiliwa nchini. 

Mwongozo wa kuandika katiba ya kikundi cha kujisaidia nchini Kenya

Katiba ni mojawapo ya mahitaji muhimu wakati wa kusajili kikundi nchini Kenya. Katiba ya kikundi inapaswa kuwa na vipengele vifuatavyo:

Kifungu cha 1: Jina la kikundi, maelezo yake ya mawasiliano na eneo lake halisi.

Kifungu cha 2: Malengo -Taja malengo ya kikundi.

Kifungu cha 3: Uanachama - Onyesha mahitaji ya kujiandikisha kama mwanachama, kujiuzulu, kurejeshwa (kujiunga tena na kikundi) na jamaa wa karibu wa wanachama wa kikundi.

Kifungu cha 4: Viongozi wa kikundi - orodhesha viongozi wa kikundi ukiionyesha majina na vyeo vyao. Vyeo muhimu zaidi ni ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu, Makamu katibu na Mweka Hazina.

Kifungu cha 5: Kazi za maafisa - Onyesha majukumu na wajibu wa kila kongozi ili waelewe kazi yao inahusisha nini.

Kifungu cha 6: Muda wa kukaa madarakani kwa viongozi - Onyesha ni muda gani viongozi watashikilia nyadhifa zao.

Kifungu cha 7: Fedha - Onyesha vyanzo, usimamizi, na matumizi ya fedha za kikundi.

Kifungu cha 8: Mikutano - Onyesha aina ya mikutano na idadi ya chini ya watu wanaohitajika ili mikutano ya kikundi ifanyike.

Kifungu cha 9: Uchaguzi - Onyesha jinsi maafisa wa kikundi watakavyochaguliwa kwa mfano, kura ya siri, kupanga safu, kunyoosha mikono, kupongeza, n.k.

Kifungu cha 10: Utunzaji wa kumbukumbu–Onyesha rekodi za kikundi zitakazowekwa na kusimamiwa.

Kifungu cha 11: Nidhamu - Onyesha kanuni za kikundi na hatua za kinidhamu zitakazochukuliwa ikiwa sheria hizi zitavunjwa.

Kifungu cha 12: Marekebisho ya katiba - onyesha mchakato unaopaswa kufuatwa wakati wa kufanya mabadiliko yoyote kwenye katiba ya kikundi.

Kifungu cha 13: Ukaguzi - Onyesha taratibu ya kufanya ukaguzi wa shughuli na fedha za kikundi.

Kifungu cha 14: Utatuzi wa migogoro - Onyesha mbinu za kuripoti migogoro na taratibu za kutatua migogoro na kuteua mpatanishi ambaye atatumiwa na kikundi.

Ibara ya 15: Uvunjaji wa kikundi - Onyesha taratibu zinazopaswa kufuatwa ili kuvunja kikundi, na jinsi mali na madeni au mikopo yatashughulikiwa.

Kifungu cha 16: Kupitishwa kwa katiba - Onyesha taratibu za kukubalika kwa katiba ya kikundi, kwa mfano kupitia mkutano.

Anwani muhimu za mawasiliano 

Wizara ya Kazi na Ulinzi wa Jamii, Idara ya Serikali ya Ulinzi wa Jamii inapatikana katika Nyumba ya Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwenye Barabara ya Bishop, mkabala na Idara ya Usajili wa Raia na Nyumba ya Wageni ya ACK jijini Nairobi. Ofisi hiyo inaweza kufikiwa kupitia:

 • Nambari ya simu: +254 2729800
 • Barua pepe: ps@socialprotection.go.ke or info@socialprotection.go.ke.  
 • Tovuti: www.socialprotection.go.ke

Vikundi vilivyojumuishwa vya wakimbizi vinasaidiwa na mashirika kusajili vikundi vyao vya kujisaidia. Hizi ni:

KAKUMA
ORGANIZATIONLOCATIONCONTACTS
Norwegian Refugee Council (NRC)Ofisi za NRC, kando ya Ofisi za UNHCR.

Nambari ya Ofisi ya Taarifa, Ushauri na Usaidizi wa Kisheria (ICLA): 0703503744 

Nambari ya Simu ya bure ya NRC Kakuma: 088721788  

NAIROBI
International Rescue Committee (IRC)

1. Kituo cha Rasilimali za Maisha (LRC) cha Pangani - Gorofa ya pili ya jumba la KCDF, Chai Road

2. Kituo cha Rasilimali za Maisha (LRC) cha Kawangware – Gorofa ya kwanza, Kivuli Center, Kabiria, karibu na  Mtaani Radio

3. Kituo cha Rasilimali za Maisha (LRC) cha Rongai – Gorofa ya 4, jumba la Tyme Arcade, Barabara ya Magadi kwenye maeneo ya Barclays.

 
Danish Refugee Council (DRC) PCEA Rev. Kareri, Eastleigh Field Office   
HIAS Kenya  HIAS Mimosa- Barabara ya Mbaruk, kando ya Muchai Drive, kando ya Barabara ya Ngong. 
Refuge Point  Titan Complex, gorofa ya pili, kwenye barabara ya Chaka, maeneo ya Hurlingham. 

Ikiwa una maswali yoyote, tafadhali tuandikie kupitia ukurasa wa Facebook wa Julisha.Info au zungumza nasi kupitia WhatsApp (+254110601820) ,Jumatatu hadi Ijumaa kutoka 08:00 asubuhi hadi 5:00 jioni