Jambo la Kuzingatia: Mnamo Oktoba 2022, serikali ya Kenya iliteua jopokazi la kukusanya maoni ya umma kuhusu utekelezaji wa Mtaala unaozingatia Umahiri (CBC) na kutoa mapendekezo. Ukusanyaji wa maoni ya umma ulihitimishwa mnamo Novemba 2022. Kwa sasa serikali inapitia matokeo ya jopokazi hilo. Mara tu mchakato huu utakapokamilika, tutasasisha makala haya ili kujumuisha mabadiliko yatakayofanywa kwenye mtaala.

Mtaala unaozingatia umahiri maarufu kama CBC unatumika kutoa mafunzo nchini Kenya na kutathmini uwezo na udhaifu wa wanafunzi. CBC ni mfumo mpya wa elimu nchini ulioanzishwa mnamo Desemba 2017. Chini ya mfumo huu, maendeleo ya kila mwanafunzi yanafuatiliwa kwa muda wa miaka 2-6-3-3, ikigawanywa  katika viwango vitatu vikuu vya elimu:  

  • Elimu ya awali (PP1 na PP2)
  • Elimu ya msingi 
  • Elimu ya shule ya upili, elimu ya juu na elimu ya chuo kikuu. 

Katika makala haya, utajifunza zaidi kuhusu mtaala wa shule za msingi ambapo wanafunzi hupata elimu yao ya miaka ya awali. Pia utajifunza zaidi kuhusu usajili na mchakato wa kutathmini,  mada za masomo, na jinsi wanafunzi walio katika ngazi hii hupewa alama. 

Kabla ya kujiunga na shule za msingi, watoto wanatarajiwa kumaliza elimu yao ya awali inayoanza wakiwa na umri wa miaka 4. Unaweza kusoma zaidi kuhusu  kuhusu mahitaji, nyenzo za kujifunzia na maeneo ya kujifunzia kwa elimu ya awali kwa kubonyeza hapa 

Wanafunzi hujiunga na shule ya msingi ya chini baada ya kumaliza miaka miwili ya elimu ya awali (PP1 na PP2). Katika shule ya msingi, masomo imegawanywa katika darasa la 1, 2 na 3. Huu ni mwendelezo wa elimu ya miaka ya mapema ya mtoto. 

mceclip0.png

Umri unaotarajiwa wa wanafunzi wa shule ya msingi. 

  • Grade 1 -wanafunzi walio na miaka sita 
  • Grade 2- wanafunzi walio na miaka saba 
  • Grade 3- wanafunzi walio na miaka minane 

Masomo yanayotolewa katika darasa la 1, 2, na 3 

  • Kusoma na kuandika au shughuli za kisomo cha breli kwa wanafunzi wenye ulemavu wa kuona (upofu) 
  • Shughuli za lugha ya Kiswahili au Lugha ya Ishara ya Kenya (KSL) kwa wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia (uziwi) 
  • Lugha ya Kiingereza 
  • Shughuli za hisabati kama vile kuhesabu 
  • Shughuli za mazingira 
  • Shughuli za usafi na lishe 
  • Elimu ya dini - elimu ya dini ya Kikristo, elimu ya dini ya Kiislamu au elimu ya dini ya Kihindu. 
  • Kusonga na shughuli za ubunifu kama vile kucheza michezo, muziki, sanaa na michezo 

Katika mwaka wa mwisho wa elimu ya msingi, wanafunzi wote wa darasa la 3 wanatarajiwa kusajiliwa na kuandikishwa kwa tathmini ya kitaifa. Walimu hufanya tathmini hiyo kwa utaratibu uliopangwa vyema unaoongozwa na Baraza la kitaifa la mitihani la Kenya (KNEC). 

Alama zote za wanafunzi waliosajiliwa kufanya tathmini hiyo hupakiwa kwenye tovuti ya baraza la kitaifa la mitihani mtandaoni. KNEC ndiyo chombo cha kitaifa chenye jukumu la kusimamia mitihani ya kitaifa nchini Kenya. Unaweza kujifunza zaidi kuhusu KNEC hapa. 

Usajili na utathmini katika shule ya msingi – wanafunzi wa darasa la 3 

Utambulisho na usajili wa wanafunzi wa darasa la 3 kwa ajili ya kutathminiwa ni wajibu wa shule na lazima ukamilishwe kwenye tovuti ya KNEC na walimu. 

Tovuti ya KNEC ya tathmini za darasa la 3 huweka data ya kibiolojia (biodata) ya kila mwanafunzi. Hii ni pamoja na: 

  • Majina rasmi ya mtoto, kwa ukamilifu jinsi yanavyoonekana katika cheti chao cha kuzaliwa 
  • Jinsia 
  • Nambari ya cheti cha kuzaliwa 
  • Tarehe ya kuzaliwa 
  • Uraia 
  • Ulemavu (kama upo) 

Baada ya tathmini ya darasa la 3 ya Kenya Early Years Assessment (KEYA) inayofanywa na KNEC, wanafunzi huanza elimu yao ya msingi ya juu katika darasa la 4. Habari zaidi kuhusu elimu ya msingi ya juu (Grade 4, 5 na 6) inapatikana hapa. 

Kuripoti na Kutoa alama kwa wanafunzi wa darasa la 3 

Tofauti na siku za awali ambapo wanafunzi walipangwa kwa kutumia alama, mfumo wa CBC hutumia mbinu tofauti kufuatilia uwezo wa mwanafunzi. Wanafunzi wa shule ya msingi ya chini hukamilisha kazi kibinafsi na katika vikundi ili kuonyesha uwezo wao. Baada ya hiyo, walimu wataangalia na kuweka kumbukumbu za jinsi kila  mwanafunzi alivyofanya kwa kuzingatia uwezo unaotokana na ushahidi. Wanafunzi watapangwa kama ifuatavyo: 

  1. Kuzidi matarajio - Alama ya juu zaidi inayotolewa wakati mwanafunzi anafanya kwa usahihi au kukamilisha shughuli zote kama inavyotarajiwa katika kila somo 
  1. Kutimiza matarajio - Mwanafunzi anafuata maagizo kwa usahihi; hufanya kazi ipasavyo na hukamilisha shughuli nyingi katika kila somo. 
  1. Kukaribia matarajio - Mwanafunzi hujaribu kufuata maagizo lakini huwa hakamilishi kazi au shughuli katika kila somo. 
  1. Chini ya matarajio - ambapo mwanafunzi anaonekana kuwa na dosari kubwa au kutoweza kukamilisha kazi kama alivyoagizwa na mwalimu. 

Ada za mitihani ya kitaifa ya darasa la 3 

Serikali ya Kenya hulipa ada zote za mitihani kwa tathmini ya KEYA kwa wanafunzi wa raia wa Kenya katika  darasa la 3. UNHCR na mashirika mengine inayosimamia mashule katika kambi za wakimbizi hulipa ada hizo za wanafunzi wakimbizi. 

Utakachotarajia kutoka kwa mtoto baada ya kumaliza elimu ya msingi. 

  • Kufikia mwisho wa elimu ya msingi, mtoto anapaswa kuwa na uwezo wa: 
  • Kuthamini kazi za sanaa, muziki na harakati zake na za wenzake kutoka zamani hadi sasa ndani ya muktadha na tamaduni zao za kijamii. 
  • Kueleza  mawazo, hisia na tajriba kupitia kazi za sanaa, muziki na utendaji. 
  • Kukuza  hali ya kujiamini na hisia ya mafanikio kupitia kutengeneza na kuthamini kazi za sanaa, muziki na utendaji wa kibinafsi na za wenzake. 
  • Kuunda kazi za kisanaa, kutumbuiza na kutumbuiza ili kubadilishana mawazo, maoni, hisia na uzoefu wao kwa ajili ya kujifunza na kufurahia. 
  • Kutumia lugha ifaayo katika kuthamini kazi za sanaa, muziki na harakati kwa mawasiliano na ushirikiano. 
  • Kutii sheria na ku shirikiana na wengine ili kutimiza majukumu ya kibinafsi huku akizingatia ipasavyo afya na usalama wake. 

Unaweza kusoma zaidi kuhusu mtaala wa elimu ya msingi ya chini kwenye tovuti ya Kenya Institute of Curriculum Development (KICD) kwa kuzungumza na walimu shuleni. 

Ikiwa una maswali yoyote, tafadhali tuandikie kupitia ukurasa wa Facebook wa Julisha.Info au zungumza nasi kupitia WhatsApp (+254110601820), Jumatatu hadi Jumamosi kutoka 08:00 asubuhi hadi 5:00 jioni