Kifua kikuu ni nini?

Kifua kikuu (TB) ni ugonjwa wa kuambukiza ambao huathiri zaidi mapafu (TB ya mapafu), ingawa inaweza pia kuathiri viungo vingine kama vile ubongo, ini, figo na mgongo pia (TB ya ziada ya mapafu). TB Inazuilika na inatibika.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), TB inaambukiza watu milioni 10 na huua watu milioni 1.5 kila mwaka, na hivyo kuifanya kuwa muuaji wa pili wa magonjwa ya kuambukiza baada ya Covid-19.

Nchini Kenya, inakadiriwa kuwa watu 139,000 walipata TB mwaka 2020, huku watu 21, 000 wakifa kwa sababu ya ugonjwa huo mwaka huo. Unaweza kusoma zaidi kuhusu TB nchini Kenya katika ripoti hii.

TB inaenezwa vipi?

Bakteria wanaosababisha TB huenezwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kupitia matone madogo madogo ambayo hutolewa hewani wakati mtu ambaye ameambukizwa TB anakohoa, kupiga chafya, kuzungumza, kutema mate, kuimba au kucheka.

SWA_TB_Transmission.png

TB inaweza kuwa hai au isiyo hai/iliyofichika. Ukipumua vijidudu vinavyosababisha TB na kuugua unakuwa na TB hai, ambayo pia hujulikana kama ugonjwa wa TB. Mtu aliye na TB hai anaweza kueneza ugonjwa huo. Kuwasiliana kwa karibu kwa muda mrefu na mtu ambaye ana ugonjwa wa TB huongeza uwezekano wa kuambukizwa ugonjwa huo.

Kwa upande mwingine, kuwa na TB isiyo hai au iliyofichika, ina maana kwamba ulikuwa umeambukizwa na vijidudu vinavyosababisha TB, lakini mwili wako uliweza kukabiliana nayo na haukua mgonjwa. Watu wenye TB isiyo hai hawana dalili za ugonjwa huo na hawaenezi ugonjwa huo. Hata hivyo, ikiwa kinga yao itadhoofika, wanaweza kupata ugonjwa wa TB.

Nani anaweza kupata ugonjwa wa TB?

Watu ambao wako katika hatari kubwa ya kupata TB ni pamoja na:

  1. Watu walio na kinga ya chini ikiwa ni pamoja na:

-watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi

- watu walioathirika na mambo kama vile utapiamlo, kisukari, wagonjwa wa saratani, ulevi wa kudumu, na kuvuta sigara.

  1. Watu ambao wamekuwa na uhusiano wa karibu kwa muda mrefu na mtu ambaye ana TB hai.

Ishara na dalili za TB hai:

  • Dalili na ishara kawaida za TB hai ni pamoja na:
  • Kukohoa
  • Kukohoa damu
  • Kutokwa na jasho usiku (mtu anapoamka akiwa amelowa jasho)
  • Maumivu ya kifua, au maumivu wakati wa kupumua na kukohoa
  • Kupoteza hamu ya kula
  • Kupunguza kilo bila sababu
  • Kuhisi uchovu mara kwa mara au udhaifu wa jumla
  • Kuhisi joto isiyo kawaida
  • Kukosa pumzi

TB inaweza pia kuathiri sehemu nyingine za mwili wako mbali na mapafu. Wakati hii itatokea, ishara na dalili zitakuwa tofauti kulingana na viungo ambavyo vitaathirika. Kwa mfano, TB ya figo inaweza kusababisha uwe na damu kwenye mkojo wako, au TB ya utando unaozunguka ubongo (TB meningitis) inaweza kusababisha maumivu ya kichwa na kuchanganyikiwa.

Matibabu

Matibabu ya TB inatolewa BURE katika vituo vya afya vya umma nchini Kenya, ikijumuisha vituo vyote vya afya katika kambi za wakimbizi za Kakuma na Hagadera.

Vituo vya afya katika Kambi ya Kakuma

Kituo cha Afya

Eneo inapopatikana

Kaapoka Health Centre / Main Hospital

Kakuma 1

Lochangamor Dispensary / Clinic 4

Kakuma 1

Hong-Kong Dispensary / Clinic 2

Kakuma 2

Nalemsekon Dispensary/ Clinic 5

Kakuma 2

Nationokor Dispensary / Clinic 6

Kakuma 3

Ammusait General Hospital /IRC General Hospital

Kakuma 4

Natukubenyo Health Center / Kalobeyei Health centre

Kalobeyei V1

Naregae Dispensary/ Kalobeyei Village 2 Clinic

Kalobeyei V2

 

Vituo vya afya katika Kambi ya Dadaab

Kituo cha Afya

Eneo Inapopatikana

Red Cross

Ifo Camp 

MSF Hospital

Dagahaley Camp

Hagadera refugee camp hospital

Hagadera refugee camp

 

Ni muhimu kuenda hospitalni  ikiwa unapata mojawapo ya dalili zilizoorodheshwa hapo juu. Unapaswa pia kwenda hospitali ikiwa umewasiliana na mtu ambaye amepimwa na akapatikana kuwa na TB.

Maambukizi ya TB na ugonjwa wa TB yanatibika.

Ikiwa una maambukizi ya Kifua Kikuu (TB), daktari wako anaweza kukushauri unywe dawa kabla haijaanza kuwa ugonjwa waTB.

Matibabu ya Kifua kikuu hai huhusisha unywaji wa madawa kwa muda usiopungua miezi sita. Ikiwa unafuata maagizo ya daktari wako na kuzingatia dawa hizi, unaacha kusambaza ugonjwa huo baada ya wiki chache.

Kutibiwa kwa TB kutakusaidia kupata nafuu na kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo kwa wengine. Iwapo utathibitishwa kuwa na TB hai, unashauriwa kufuata vidokezo hivi ili kuwaweka salama wale walio karibu nawe:

  • Kaa nyumbani katika wiki chache za kwanza za matibabu. Iwapo huwezi kukaa nyumbani, jaribu kuweka umbali kati yako na watu wengine na:
  • Vaa barakoa (face mask) ukiwa karibu na watu wengine.
  • Funika mdomo wako na kitambaa unapokohoa, unapopiga chafya, au kucheka, kisha tupa kitambaa hicho kwenye choo cha shimo.
  • Hakikisha kuwa vyumba vyako vina mtiririko wa hewa. Bakteria wanaosababisha TB huenea kwa urahisi zaidi katika maeneo yaliyofungwa ambayo hayana mtiririko wa hewa.

Most importantly, ensure you FINISH your medication. When you stop taking the medication or skip doses, the TB bacteria mutates (changes) and develops a resistance to the drugs. Cha muhimu zaidi, ni unafaa kuhakikisha kuwa UMEMALIZA dawa zako. Unapoacha kutumia dawa au kuruka dozi, bakteria wa TB hubadilika na kukuza ukinzani kwa dawa.

Chanjo

Watoto wote wanaozaliwa nchini Kenya hupokea chanjo ya Bacille Calmette-Guerin (BCG) mara tu baada ya kuzaliwa. Chanjo ya BCG humlinda mtoto wako dhidi ya aina kali za TB, ikiwa ni pamoja na TB ya uti wa mgongo. Chanjo inatolewa kama sindano kwenye mkono wa kushoto wa mtoto na kuacha kovu. Akina mama wote wanapaswa kuhakikisha kwamba watoto wao wanapata chanjo hii kabla ya kutoka hospitalini baada ya kujifungua. Chanjo hiyo inatolewa bila malipo katika vituo vyote vya afya vya umma vya Kenya pamoja na vituo vya afya kote kambini.

Ikiwa una maswali yoyote kuhusu ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) na matibabu yake, wasiliana nasi kupitia ukurasa wa Facebook wa Julisha.Info, Jumatatu hadi Ijumaa kutoka saa mbili asubuhi (08:00 a.m.)  hadi saa kumi na moja jioni (5:00 p.m)