KPL_PHOTO1.jpeg

Wachezaji wa Ligi Kuu ya Kakuma wakicheza katika mechi iliyopita ya soka. Vijana katika kambi wamekubali ligi hiyo kama njia ya kuzidisha kuishi kwa Amani na usawa kambini. [Picha / LWF-Kakuma}

Uwezo wa kipekee ya michezo unaweza kubadilisha maisha na ulimwengu katika muda mfupi zaidi, ni onyesho la kweli kabisa la yote yanayowaleta watu pamoja. Huko Kakuma, vijana na viongozi hutumia michezo kuwasiliana na kuangazia mamboa yanayoathiri maisha yao ya kila siku.

Huku dunia nzima ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Vijana ya 2021, Julisha.Info inaangalia jinsi soka imewapa matumaini na motisha vijana wengi katika Kambi ya Wakimbizi ya Kakuma.

Ingawa wanakabiliwa na changamoto nyingi na hali ngumu ya maisha kambini, pamoja na uhaba wa chakula na maji safi, magonjwa, uhalifu, ukosefu wa nafasi na joto kali sana, vijana wengi wanashabikia Ligi Kuu ya Kakuma (KPL).

Vijana wengi wamepata faraja kwa kucheza soka kambini. Mwangaza ambao soka huleta kwenye kambi ni zaidi ya mawazo ya wote.

Ligi hiyo iliyoanzishwa mnamo 2016 na mpango wa Ulinzi na Maendeleo ya Vijana wa Shirikisho la Kilutheri la Ulimwenguni (LWF) inawapa vijana wengi ndoto na jukwaa la kuonyesha talanta zao katika  soka.

Mechi ya kwanza ya ligi hiyo ilichezwa katika uwanja wa Virunga huko Kakuma 3 zone 2 mnamo Juni 30, 2016, na siku hiyo hiyo timu ya wanariadha 5 wakimbizi kutoka Kakuma ilikuwa huko Rio nchini Brazil ikijiandaa kushiriki michezo ya Olimpiki ya Rio ya 2016.

Miaka kadhaa baadaye, mashindano hayo yamewapa vijana wengi kitu cha kutazamia, kuotea na kufanyia kazi kwa bidii. Hivi sasa, timu 16 zinashiriki kwenye ligi.

Timu hizo ni pamoja na: Okapi FC, Virunga United, Lamasia, Tarachi, Kakuma Rangers, Fizi, Shambe, Equatorial, Nuer Boys, Dinka All Stars, 99 Mountains, Ochuok, Kadar, Kinati, Naath Boys na Dinka Legends.

Ili kuhakikisha kuwa wasichana pia wanahusika katika shughuli za michezo, LWF pia inaendesha ligi ya wasichana inayojulikana kama Ligi ya Kakuma Divas (KDL).

Wasichana 300 wanashiriki kwenye ligi hiyo. Ligi ina timu 10 zilizotolewa kutoka kambi za Kakuma, makazi ya Kalobeyei na jamii ya wenyeji/watoa hifadhi kwa wakimbizi.

Msichana wa miaka 17, Emmanuella Biluge, aliyejiunga na ligi ya wasichana baada ya kufanya mitihani yake ya darasa la nane mnamo 2020, anasema kuwa kucheza kwenye Ligi ya Divas ya Kakuma ni kama ndoto kutimia.

“Ninapenda mpira wa miguu na ndiyo sababu nilijiunga na Talanta FC kucheza katika KDL. Kucheza hunisaidia kujiweka sawa na kuwa na bidii wakati sipo shuleni. Kupitia ligi hiyo, nimepata nafasi ya kushirikiana na watu wengine wa mataifa tofauti. Natumai kuchezea timu kubwa ulimwenguni siku moja,”Biluge alisema.

Licha ya kuwa mwanafunzi katika shule ya Sekondari ya Kakuma, msichana huyo wa kidato cha kwanza hutenga wakati baada ya masaa ya shule kufanya mazoezi na wachezaji wenzake.

Je! Mtu anawezaje kujiunga na timu katika KPL, KDL?

Ligi hiyo inafuata sheria za FIFA ambapo timu mbili za mwisho kwenye jedwali la ligi hushushwa na kubadilishwa na timu zingine mbili kila mwisho wa msimu.

Mashindano huandaliwa na LWF mwishoni mwa msimu ambapo timu mbili bora hupata kupandishwa hadi Ligi Kuu ya Kakuma (KPL). Timu zote zisizo za KPL zinaruhusiwa kushiriki mashindano haya.

Ili kustahiki kujiunga na ligi hiyo, timu lazima iwe na wachezaji kutoka mataifa tofauti / kabila nyingi. Timu hufanya mazoezi jioni katika uwanja unaopatikana kwenye kambi. Kujiunga na timu ni bure, unahitaji tu kujitokeza kwa mazoezi na kumfurahisha kocha.

KPL_PHOTO2.jfif

Mashindano ya zamani ya Ligi Kuu ya Kakuma. Wanaoangalia ni mashabiki wa soka kutoka kambi ya wakimbizi, jamii ya wenyeji na eneo la makazi ya Kalobeyei. [Picha / LWF-Kakuma}

Kukuza talanta ya soka na ubora

Wachezaji bora na wafungaji bora katika ligi wanachukuliwa kama watu mashuhuri katika jamii na wamepewa majina ya utani kama ya wachezaji maarufu wa soka kama "Dinho", "Messi" na "Cristiano".

Kupitia ligi hiyo, vijana wa wakimbizi ambao mara chache wanapata fursa ya kutokanje ya kambi, sasa wana nafasi ya kutoka kambini na kucheza na timu za Ligi Kuu ya Kenyab(FKFPL) na ligi zingine bora ulimwenguni.

Ligi hiyo hadi sasa imezalisha wachezaji wawili ambao wanachezea katika Klabu ya Soka ya Nzoia United ya Ligi ya Soka Kenya (FKFPL). Wawili hao, Gaetan Masha na Felix Okanda, walichezea Virunga United na Okapi FC mtawaliwa kabla ya kutafutwa kujiunga na Nzoia FC.

Wanasoka hawa wawili ni mfano wa kuigwa kwa wachezaji wachanga ambao huenda kwenye uwanja wenye vumbi kwenye jua kali kila wikendi wakitumaini kuwa siku moja watapata fursa hiyo.

Bukuru Christopher Asumani, maarufu kwa jina la utani la soka "Vich", amekuwa akicheza soka kambini kwa miaka mitano tangu amalize masomo yake ya kidato cha nne mnamo 2015.

Asumani ni mmoja wa wachezaji ambao wamebahatika kuchaguliwa kutoka kwenye ligi hiyo kujiunga na Timu ya Soka ya Kakuma United ambayo inacheza kwenye ligi za mkoa wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF).

“Nilipomaliza kidato cha nne mwaka 2015, sikuwahi kufikiria kuw nitapata nafasi ya kuichezea Kakuma United. Nilikuwa nikichezea Okapi FC wakati nilitafutwa kujiunga na Kakuma United. ” Asumani alisema.

Kukuza uwepo wa amani katika kambi na mshikamano.

Kuwa mchezo unaopendwa zaidi na vijana wengi wa wakimbizi, KPL imekuwa ishara ya umoja, amani na upendo kwa wakimbizi na jamii inayotoa hifadhi kwao.

Mashindano haya yanawaleta pamoja jamii zinazoishi katika kambi hiyo na jamii inayotoa hifadhi, na kukuza mshikamano. Kati ya timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo, mbili ni kutoka kwa jamii ya wenyeji.

“Kucheza soka ni muhimu kwangu. Ninafurahia, inanifanya niwe na nguvu ya mwili, na inaunda fursa za kazi. Pia huleta watu pamoja; sasa tunaweza kushirikiana kama vijana bila kujali asili yetu ya kabila” Asumani alisema.

Mechi za ligi hiyo zimekuwa mambo makubwa ya kijamii kambini na huvutia maelfu ya wapenda soka ambao wanajitokeza kila wikendi ili kushangilia timu na wachezaji wanaowapenda.

Njia ya kukuza uelewano kuhusu maswala yanayoathiri jamii

Viongozi wa jamii hutumia mechi hizo kupitisha habari muhimu kambini zaidi wakati wa janga hili la COVID-19.

Kutumia soka, wadau katika sekta ya afya wanachukua fursa ya mashindano hayo ili kuongeza uelewano kuhusu jinsi ya kukomesha kuenea kwa virusi katika jamii.

Wadau wameshirikiana na timu hizi kuweka vyombo vya kunawa mikono kambini. Timu hizo pia hushiriki katika shughuli za kawaida za usafi katika kambi.

Asumani, mkimbizi wa Kongo, anatumai kuwa siku moja atacheza mpira wa miguu na kupitia KPL atafuata nyayo za Gaeten Masha na Felix Okanda.

Yeye hatarajii tu kucheza Ligi Kuu ya Kenya, lakini pia kujiunga na ligi bora ulimwenguni.

Hata tunapojitokeza kwa idadi kushangilia na kufurahiya mechi, kumbuka kujilinda, familia, na marafiki dhidi ya COVID-19 kwa kuzingatia itifaki za WHO.

Kumbuka:

  • Vaa barakoa yako vizuri.
  • Epuka kugusa mdomo na pua.
  • Tembea na “sanitizer” iliyo na kiwango cha kileo cha asilimia 60 na uitumie mara nyingi.
  • Funika mdomo na pua unapokohoa na upige chafya kwenye kiwiko lako.

Kwa maelezo zaidi kuhusu unavyoweza kujilinda na familia kutoka kwa COVID-19 soma nakala hii.

Ligi Kuu ya Kakuma inadhaminiwa na LWF kwa kutoa usafiri pale inapohitajika, kufanya mipango ya usalama, kusaidia sekretarieti ya ligi, tuzo na usimamizi wa tuzo, usimamizi, na uwajibikaji wa msaada wa vifaa na kifedha.

Je! Ungependa kushiriki michezo huko Kakuma? Tafadhali tuandikie kupitia ukurasa wa Facebook wa Julisha.Info, Jumatatu hadi Ijumaa kutoka saa 2 asubuhi hadi saa 11 jioni.